Saturday, June 30, 2012

Vyombo vya habari vyatakiwa kuepuka habari za kuchonganisha

Vyombo vya habari vimetakiwa kuwa makini na kuepuka kuandika habari zinazohusu imani za kidini kwa kuegemea upande mmoja ama  kwa majumuisho ili kuepusha  kuchochea chuki miongoni mwa jamii.
“ Jambo hilo ni muhimu siyo tu  kwa manufaa ya taaluma  bali pia  kwa kulinda amani na umoja  katika Taifa’, Katibu Mtendaji  wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga aliwaambia waandishi wa habari  mjini Dar es Salaam leo.
Mukajanga, alisema kuwa kumeibuka  uandishi  usiozingatia  uhalisia, ulinganishi na umahususi badala yake  uandisi unachukua mfumo wa kuegemea upande mmoja  na kufanya majumuisho yasiyotokana na  ukweli uliothibitishwa na mwandishi.
“Mapungufu hayo ya kiweledi”, alisema, “yamesababisha habari nyingi kuwa potofu na chonganishi”.
Alisema kuwa weledi hautaki  kwa mfano gazeti kumhoji sheikh mmoja au kadhaa au askofu mmoja au kadhaa na kuandika  vichwa vya  habari vinavyosema “ Waislamu wataka….” au “ Wakristo wakata..”.
“Ikiwa yanayosemwa ni mawazo ya kiongozi mmoja wa dini ni bora isemwe hivyo. Dhehebu linaweza kuhusishwa  tu ikiwa  yeye ni msemaji rasmi na anaongea kwa niaba ya dhehebu hilo”,  alisema Mukajanga.
Vichwa vya habari kama “Maaskofu wamng’oa Naibu Meya Arusha” huku kukiwa `hakuna ushahidi wowote ndani ya habari yenyewe unaoashiria kuwa  kujiuzulu kwa  huyo Naibu Meya  kulitokana na shinikizo la maaskofu ni upotoshaji unaoweza kusababisha chuki, amesema Mukajanga.
Mbaya zaidi, Mukajanga alisema,  ni pale  kesho yake gazeti jingine  linapowatafuta masheikh  na kuwaomba kauli  yao kuhusiana na  kung’olewa kwa Naibu Meya kulikofanywa na  maaskofu.
“Ni wazi hapa kuna hatari ya  ya wanahabari kugeuka wachonganishi”, alisema Mukajanga.
Pia  alisema kumewahi kuchapishwa kichwa kilichosema “ Masheikh wawaonya maaskofu”. Hii ni hatari,  alisema.
Mukajanga pia  alisema  habari nyingine ilidai bila  uthibitisho wowote kuwa waumini wa Kanisa Katoliki wametengwa na Kanisa hilo kwa kujihusisha na chama fulani cha siasa. Viongozi wa kanisa  hilo hawakuhojiwa, alisema.
Hivi karibuni, Mukajanga  alisema, gazeti moja liliandika “Waislamu: Osama hajafa – wadai kuzikwa haraka ni  dalili za kuficha ukweli”.
Mukajanga alihoji hivi ni  kweli maoni kwamba Osama  hajafa yalikuwa maoni ya waislamu wote nchini?
Pia aliuliza baada ya  Al-Qaeda wenyewe  kukiri kuwa Osama kafa, gazeti hilo  halikusikia vibaya kwamba limewasababishia dhihaka Waislamu wote bila uhalali wowote lilipowasingizia kwamba wamesema Osama hajafa?
Gazeti lingine, Mukajanga alisema lilimnukuu mchungaji mmoja  aliyepinga  ukaguzi wa mahesabu  ya makanisa na kuandika  kichwa cha habari  kilichosema “Makanisa yakataa kukagulkiwa na serikali”.
Hata hivyo  Mukajanga alisema, baadaye  katibu wa makanisa hayo  yaliyotajwa  alinukuliwa akisisitiza kuwa yale yalikuwa mawazo binafsi ya mchungaji huyo.
Mukajanga alinukuu kifungu cha  1.9 cha kanuni za  maadili kwa wahariri (uk5) kuzuia ubaguzi kinachosisitiza: Hakikisha  habari hazilengi  wala kutoa nafasi kwa ubaguzi wa kijinsia, dini makundi ya watu wachache, umri, kabila…”
Kuhusu dini , alisema, kifungu 1.14 (uk6) kinaelekeza: Zungumza na mashrikia  ya dini, yape haki sawa na heshima yanayostahili kwani hadhi za wawakilishi, viongozi, waumini na imani zao zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
mwisho

No comments:

Post a Comment